Hub for education news and events

SHULE TANO ZA KITAIFA ZANASWA KATIKA WIZI WA MITIHANI

Waziri wa Elimu Jacob Kaimenyi akihutubu alipokuwa akitoa matokeo ya mtihani wa KCSE ya 2014 jumba la Mitihani, Nairobi Machi 3, 2015. Picha/BILLY MUTAI 

MATOKEO ya watahiniwa  2, 975 waliofanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KSCE) mwaka uliopita yamefutiliwa mbali kwa sababu ya udanyanyifu, kwa mujibu wa Waziri wa Elimu Prof Jacob Kaimenyi.

Akitangaza matokeo rasmi ya KCSE 2014, Prof Kaimenyi alisema kuwa visa hivyo vilihusisha watahiniwa kutoka shule tano za kitaifa. Aidha Waziri huyo alisema kuwa visa hivyo vimepungua kutoka 3,812 mwaka wa 2013.

Prof Kaimenyi alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa shule za hadhi ya juu kimasomo ndizo zinajihusisha na visa vya udanganyifu na kuhatarisha viwango vya elimu nchini. “Shule za kiwango cha Kaunti (County schools) pamoja na zile za kaunti ndogo (sub county) zilikuwa na idadi kubwa ya visa vya udanganyifu,” alisema Prof Kaimenyi akiwa Mitihani House, Jumanne.

Japo hakutangaza majina, alisema kuwa ilikuwa aibu sana kwa shule tano za kitaifa kujihusisha na udanganyifu licha ya kusajili wanafunzi waliofanya vyema zaidi kutoka shule za msingi.

“Nashangaa kwa nini shule ya kitaifa inachukua wanafunzi waliofanya vyema zaidi KCPE na bado inajihusisha na visa vya udanganyifu wa mtihani wa kitaifa. Wanafunzi wa shule nyingine watafanya nini nao kama wenzeo wa shule za hadhi ya juu wanadanganya?” alishangaa Prof Kaimenyi.

Alisema kuwa uhalifu huo unazidishwa na ukweli kuwa walimu wakuu wa shule na maafisa wa mitihani ndio wanaoongoza kutekeleza visa hivyo.Waziri huyo alielezea kutamaushwa sana na hatua ya walimu kuongoza wanafunzi kujihusisha na udanganyifu wa mitihani badala ya kuwa kielelezo chema.

“Wanafunzi hao wataishi maisha ya udanganyifu. Hawatawahi kuwaamini walimu tena. Ujasiri wao maishani umeathiriwa pakubwa,” alisema Prof Kaimenyi. Kulingana na Baraza la Kitaifa la Mitihani nchini(Knec), idadi kubwa zaidi ya visa vya udanganyifu inahusisha njama ya walimu na wanafunzi.

Matokeo kufutiliwa mbali

Baadhi ya wanafunzi walikiuka marufuku ya kutumia simu za mkononi na wakapatikana nazo katika vyumba vya kufanyia mitihani na kupelekea matokeo yao kufutiliwa mbali.

Maafisa wa mtihani walinasa rununu 179 katika vyumba vya kufanyia mitihani, ushahidi kamili kuwa walikiuka maagizo ya Knec. Kulingana na Prof Kaimenyi walifanikiwa kuingia katika vyumba vya kufanyia mitihani na karatasi walizoandika majibu.

Kulingana na matokeo ya 2014 ni kaunti saba pekee ambapo hakuna hata kisa kimoja cha udanganyifu kiliripotiwa.aunti hizo ni pamoja na Taita Taveta,Tana River, Lamu, Nyandarua, Marsabit, Siaya na Nyamira. Hii ni mara ya pili Kaunti za Lamu naTaita Taveta hazijahusishwa katika visa vya udanganyifu.

Powered by Bullraider.com
You are here: Home Education news SHULE TANO ZA KITAIFA ZANASWA KATIKA WIZI WA MITIHANI