Hub for education news and events

WANACHUO 150 WALAZWA BAADA YA KULA CHAKULA CHENYE SUMU

Kulingana na barua kutoka kwa chuo hicho, waathiriwa wote ni wanafunzi wa Mwaka wa Nne waliohudhuria hafla ya chakula cha jioni chuoni humo.“Hii ni kuwajulisha kuhusu kisa cha kusikitisha cha Ijumaa Machi 20, ambapo wanafunzi wetu wa Mwaka wa Nne na wafanyakazi wetu waliohudhuria hafla ya chakula cha jioni kwa wanafunzi wakuu waliathirika baada ya kula chakula hicho,” ukasema ujumbe uliotumwa na afisa wa uhusiano mwema wa chuo hicho, Bi Betty Ngala.

“Chuo Kikuu kimethibitisha jambo hili na kimechukua hatua kuhakikisha afya na usalama wa wanafunzi wote na walimu wao,” ukasema ujumbe huo.Duru zilisema kuwa baadhi ya wanafunzi wamelazwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi wakiwa wamepoteza maji mengi mwilini.

Kuna ripoti kuhusu kuathiriwa kwa figo za wanafunzi wote kwa kuwa wote wanaonyesha dalili sawa ingwa kiwango cha athari hizo za figo kinatofautiana kulingana na kiasi cha maji ambacho kila mmoja alipoteza mwilini.

Taifa Leo ilifahamishwa kuwa baadhi ya wazazi wa wanafunzi walioathiriwa wanafikiria kuchukulia chuo hicho hatua za kisheria. “Ni jambo la kutia wasiwasi kwa sababu hatujui shida tunayoshughulikia na uvumi unaosambazwa ni mkubwa,” akasema mmoja wa wazazi.

Chuo hicho hakijatoa jina la kampuni iliyotayarisha chakula hicho lakini kimesema kilitoka nje na kuwa uchunguzi umeanzishwa kuthibitisha sababu kamili ya chakula hicho kuwadhuru waliokila.Sampui za chakula na matokeo ya uchunguzi wa wagonjwa vimekusanywa na kupelekwa kwa Taasisi ya Utafiti wa Madawa (Kemri) kwa uchunguzi zaidi.

“Chuo kinafanya kinajitahidi kufahamu idadi kamili ya wanafunzi walioathiriwa,” akasema Bi Ngala. Mzazi wa mmoja wa wanafunzi walioathiriwa alisema idadi ya waathiriwa inakisiwa kuwa zaidi ya 150.

Kudhuru haraka

Mmmoja wa wanafunzi hao, Kammie Mutegi, alilaumu chuo hicho akisema hakishughuliki na ubora wa baadhi ya mambo kama vile lishe kama kinavyofanya katika masomo.

“Nimesikitishwa na kukerwa na uzembe wa chuo. Kinafaa kuonyesha uwajibikaji wa hali ya juu kama kinavyofanya katika masuala ya masomo. Kampuni iliyopewa jukumu la kutupikia chakula bila shaka ilikuwa na nia ya kutuua. Unawezaje kueleza hali kwamba kwa siku mbili sasa bado hatujapata nafuu yoyote?” akauliza Mutegi.

“Lakini tunamshukuru Maulana kwamba angalau tungali hai. Hiyo sumu ilifanya kazi haraka ya ajabu,” akaongeza. Mwanafunzi mwengine, Victoria Nthambi, alisema anashukuru kuwa yuko hai ikizingatiwa makali ya sumu kwenye chakula alichokula.

swahilihub.com

 

Powered by Bullraider.com
You are here: Home Education news WANACHUO 150 WALAZWA BAADA YA KULA CHAKULA CHENYE SUMU