Hub for education news and events

Benki ya Walimu yaanza kuuza hisa.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi (Elimu), Kassim Majaliwa (pichani), jana alizindua uuzwaji wa hisa za Benki tarajiwa ya Walimu (MCB) na kuutaka uongozi wake kutoruhusu ubadhirifu ili kuilinda benki hiyo.Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.

Akizindua uuzwaji wa hisa hizo, Majaliwa alisema serikali inatambua vilio vya muda mrefu, ambavyo vimekuwa vikitolewa na walimu, hivyo imefarijika na hatua yao ya kuanzisha benki hiyo chini ya chama chao (CWT) bila kutetereshwa na maneno yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya watu kwa lengo la kuwakatisha tamaa. Alisema serikali imejifunza mengi kutoka uanzishwaji wa benki hiyo, hivyo akataka iwe ni chachu ya kudumisha ushirikiano kati yao na walimu.

“Baada ya kupata benki, sasa nunueni hisa ili kupanua mtaji wa benki. Msiruhusu ubadhirifu. Muwe wahamasishaji badala ya kuwa wanaharakati. Serikali itatoa ushirikiano pale mtakapokwama,” alisema Majaliwa.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nasama Massinda, alisema iwapo wanachama wote hai 200,000 wa CWT watashiriki katika ununuzi wa hisa, idadi ya washiriki katika uwekezaji wa hisa kupitia masoko ya mitaji nchini unatarajiwa kuongezeka kwa takriban asilimia 100. Alisema CMSA imeweka miongozo ya uuzaji na ununuzi wa hisa njia ya teknolojia ya mawasiliano, ambayo imewezesha kuwapo ununuzi wa hisa kupitia simu za mkononi.

Nchemba alizitahadharisha taasisi, ambazo hazijajiandikisha kulipa kodi kwamba, serikali itatoa maelekezo ili utaratibu unaostahili uchukuliwe iwapo hatua ya kuwashawishi kufanya hivyo itashindikana.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa MCB, Herman Kessy, alisema CWT inamiliki mtaji wa Sh. bilioni 17, ambao umevuka kiwango cha mtaji wa Sh. bilioni wa kuruhusiwa kuanzisha benki nchini.

Alisema hisa za walimu, ambazo zinatarajiwa kufikia Sh. bilioni 11, zitauzwa kwa njia ya mtandao.Rais wa CWT, Gratian Mukoba, alisema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia kuwapo kwa benki ya walimu nchini, kwani ni ya kwanza kuanzishwa duniani kote.

CHANZO: NIPASHE

Powered by Bullraider.com
You are here: Home Education news Benki ya Walimu yaanza kuuza hisa.