Hub for education news and events

Wanafunzi kutumia namba moja kuzuia wanafunzi hewa

Kuanzishwa kwa mfumo wa namba maalumu ya usajili itakayotumiwa na wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi chuo ngazi ya diploma, kutasaidia kupunguza tatizo la wanafunzi hewa.
Hayo yalitangazwa jana na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) jijini Dar es Salaam.
Ofisa Mitihani wa Necta, Khalifan Kabiki alisema utaratibu huo unafuta uliokuwa unatumika zamani ambapo mwanafunzi alipewa namba mpya kila alipofanya mtihani.


Mfumo mpya, utamtambua mwanafunzi kwa namba atakayosajiliwa nayo darasa la kwanza ambayo ataitumia katika maisha yake yote ya shule na taarifa zake zote zitakuwa humo.

Kabiki alisema mfumo huo ambao utakuwa wa kielektroniki, utasaidia uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa kutoa namba maalumu itakayomtambulisha mwanafunzi katika ngazi mbalimbali za mafunzo.

“Mfumo huu utasadia katika uandaaji na utoaji wa takwimu za wanafunzi katika ngazi ya shule, wilaya, mkoa na Taifa. Pia utarahisisha ufuatiliaji wa taarifa za matokeo ya kila mwanafunzi ili kuhakikisha wadau wa elimu wanapata ufahamu wa kutosha kuhusu ufundishaji na ujifunzaji,” alisema Kabiki.

Pia, mfumo huo utasaidia katika uhamisho wa mwanafunzi ndani na nje ya mkoa, kwani namba hiyo itakuwa ina taarifa zake zote muhimu na hakutakuwa na haja ya vielelezo vingine.

Kabiki alisema tayari mfumo huo umeanza kujaribiwa katika mikoa ya Mwanza na Ruvuma, na ifikapo Desemba utaimarishwa zaidi ili kuanzia Januari uanze kutumika nchi nzima.

Katika hatua nyingine, ofisa habari wa baraza hilo, John Nchimbi alisema Necta imeboresha mfumo wa usahihishaji mitihani ya Taifa kwa kuweka wasahihishaji kulingana na idadi ya maswali kwa kila somo.

Pia, Necta walisema wameimarisha udhibiti wa wizi wa mitihani na udanganyifu kwa kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2011 hadi 2015.

“Usahihishaji wa sasa unatumia mfumo wa mnyororo kuepuka baadhi ya wasahihishaji kumkosesha mwanafunzi swali ambalo amelijibu kwa ufasaha kwa kuwa tu maswali yaliyotangulia alikuwa hajayajibu vizuri,” alisema.

Alisema mfumo wa kudhibiti wizi wa mitihani na udanganyifu umeimarishwa kutoka watahiniwa wadanganyifu 9,736 mwaka 2011 mpaka sifuri mwaka 2015 kwa elimu ya msingi. Kwa kidato cha nne wanafunzi 3,303 walifanya wizi na udanganyifu huo kwa mwaka 2011 lakini idadi hiyo imepungua mpaka wanafunzi 87 mwaka 2015.

Nchimbi alisema mfumo huo umepunguza wizi na udanganyifu kwa wanafunzi wa kidato cha sita kutoka 11 mwaka 2011 mpaka tano mwaka 2015.

Chanzo Mwananchi

Powered by Bullraider.com
You are here: Home Education news Wanafunzi kutumia namba moja kuzuia wanafunzi hewa